Saturday, March 30, 2013

SENENE HISTORY



Kwa kutumia vyanzo mbalimbalina imekuzwa na William Rutta – Kiroyera tours www.kiroyeratours.com

KUNA aina nyingi za wadudu ambao katika baadhi ya makabila hapa nchini hutumiwa kama kitoweo,na pia katika uzalishaji wa bidhaa za vyakula kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Senene ambao hupatikana kwa wingi mwishoni mwa kila mwaka, ni miongoni mwa wadudu wanaotumiwa zaidi na kabila la wahaya mkoani Kagera kama kitoweo, pengine kuliko kabila jingine unalolifahamu.

Hata hivyo pamoja na kitoweo hiki kupewa heshima kubwa na hata kuwa sehemu ya mila na utamaduni wa kabila hili,asili na chanzo cha senene limeendelea kuwa swali gumu miongoni mwa wenyeji wa mkoa huu.

Wahenga walisema ‘uzee dawa’na katika kutafuta majibu ya siri ya senene katika kabila hili,safari yangu ilinikutanisha na mzee David Zimbihile(80) aliyekuwa mbunge wa kwanza wa jimbo la Ihangiro sasa ni Muleba Kusini.

Wakati wa uongozi wake alikuwa na mvuto mkubwa kwa wapiga kura,na hadi leo anakumbukwa kama kiongozi ambaye utawala wake ulikuwa na baraka za wingi wa senene kila mwaka.
Anasema katika moja ya kampeini zake aliwahi kulalamikia kukosekana kwa mboga,na badala yake aliomba senene .Sara zake zilisikika na kuanzia wakati huo wananchi wakaendelea kumwamini huku madai ya uwezo wake wa kuleta senene yakitumika kutetea nafasi yake.
Mzee Zimbihile anasema pamoja na kupata umaarufu kupitia kitoweo cha senene miongoni mwa wapiga kura,anasema hakuwa na uwezo huo na kudai aliwaomba na Mungu akasikia sara zake kutokana na uhaba mkubwa wa mboga uliokuwepo wakati huo.
Hata hivyo pamoja na kusema senene ni kitoweo kinachoheshimika bado hakuweza kufahamu asili yake na sababu za wadudu hao kuvutiwa na mazingira ya mkoa wa Kagera katika misimu miwili kwa mwaka.
Anaamini ni uwezo na mapenzi ya Mungu,huku akikumbuka wakazi wa eneo la Bunya katika nchi ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) walivyomshanga wakati alipokuwa wanakamata na kula senene enzi hizo akifanya kazi nchini humo.
Maswali yangu hayakupata majibu na alihitimisha mazungumzo kwa kusisitiza kuwa tamaa ya kula senene iliwafanya wanaume kuwaongopea wanawake kuwa kama wangekula kitoweo hicho kingeweza kuwadhuru.
Hata nilipozungumza na Saida Sarehe(67)mkazi wa eneo la Kashai mjini hapa,alidai hakuna historia yoyote kwenye kabila lao inayoeleza chanzo na asili ya wadudu hao na kudai Mungu aliitoa kama neema kwa wakazi wa mkoa huo.
Ni muuguzi mstaafu ambaye anaishia kunisimulia jinsi wasichana wa enzi zao walivyopeleka senene kwa wachumba wao,ambaye hakufanya hivyo ilimaanisha uwezekano wa kuolewa na mchumba wake ulikuwa mdogo.Senene walitumika kama ishara ya upendo na uaminifu.
Anasema hawakuruhusiwa kula senene na kudai vitisho vya wanaume vilivyojificha kwenye tamaa na uroho wa senene viliwafanya wale kitoweo hicho kwa siri kubwa.
Bila kunipa majibu ya maswali yangu,analalamikia ubabe wa wanaume uliowakataza kula vitu vitamu na kuanzia hapo ananipa siri ya eneo la mkoa huu kuitwa Buhaya. Kuna baadhi ya vitu vitamu vingine kama kuku, nyama ya mbuzi, mayai wakina mama hawakurusiwa kula. Wazee wa kihaya kimila walidai mwanamke alikuwa haruhisiwi kutmumia vile kizazi kilikua shida na kwa kutumia mayai, nyama ya mbuzi na kuku wangenenepa na kushindwa kuzaa kwa wepesi ikawa ni mwiko, Bibi yangu Felista Nyamwiza aliyafariki mwaka 2010 akiwa namika 88 hakuwahi kula senene, yai wala kuku katika maisha yake yote pamoja na kutuandalia senene sisi wajukuu zake.
Kwamba wanawake walionywa wawe na haya siku zote, na wasivunje mwiko kwa kula vitu walivyokatazwa.Wote walikuwa na utii wakiheshimu mila na desturi za kabila lao.Walifundishwa kuwa na haya wasichana wa Buhaya.
Hata Khadija Khalphan(84)mkazi wa Kashai mjini Bukoba mbali na kufahamu umuhimu na nafasi ya kitoweo cha senene katika mila za kabila lake anakiri kutofahamu chanzo na asili ya wadudu hao.
Hata mvua za vuli zinazoanza mwezi Novemba ambazo huambatana na ujio wa senene ,msimu huo hutambuliwa na wenyeji kwa jina la mvua za Omusene ikiwa na maana halisi ya mvua za msimu wa senene.
Pamoja na senene kuwa ishara ya neema katika kabila hili,pia inadaiwa ni dalili za kuwepo tukio baya endapo mtu ataota kuona senene wengi.
Juhudi za kufahamu siri ya senene zinanifikisha katika kituo cha Utafiti wa Kilimo Maruku,na baada ya kushindwa kumpata mtaalamu wa sayansi ya wadudu niliamua kutafuta majibu kwenye vyanzo mbalimbali kwenye mtandao wa intaneti.
Zipo aina nyingi za senene ambapo wale ninaowazungumzia wamegawanyika katika kundi lijulikanalo kwa kitaalamu kama Orthopterous na huzaliana kwa wingi katika mwambao wa maziwa makuu,baada ya kutaga mayai yao ardhini kipindi cha kiangazi.
Baada ya kutaga mayai na kuanguliwa,mzunguko wa maisha yao huisha kati ya mwezi Octoba na Desemba ambapo huruka wakiwa katika makundi makubwa wakihitimisha safari ya maisha yao.
Senene hao ambao wako katika jamii ya nzige pia hutofautiana kutegemea mazingira yaliyopo na hali ya hewa, na tangu zamani hupenda kuweka makazi yao juu ya vilima.
Kwa mujibu wa vyanzo vya mtandao katika nchi ya Japan senene wa kijani humaanisha dalili njema,na mwanzo mzuri wenye matumaini ambapo pia hutumika katika utengenezaji wa chokoleti.
Hii ni aina ya panzi wapole ambao hawana tabia ya kuharibu mazao na kuteketeza makazi yao kwa chakula kama walivyo jamii ya nzige.
Hawa ni aina ya panzi ambao baada ya kuzaliana, maisha yao ya mwisho hupenda kuyamalizia kwenye ukanda wa kijani na bila shaka mkoa wa Kagera ukiwa ni chaguo bora zaidi.
Senene huanza safari yao wakati wa giza huku pembe zao zikiwa zimeangalia chini na mara waonapo mapambazuko hujificha chini kwenye nyasi.
Pengine ndiyo sababu wafanya biashara wa senene hufanikiwa kuwahadaa kwa mwanga mkali wa taa,na mara kadhaa makundi makubwa ya senene huletwa na mawimbi ya maji baada ya mapambazuko kuwakuta kwenye maeneo ya ziwa Viktoria.
Senene hupatikana mahali pengi duniani ingawa hutofautiana kutokana na mazingira na ikolojia ya eneo hilo.Madume hutoa mlio maalmu kuwavutia majike ingawa pia milio hiyo hutofautiana kutokana na aina ya senene na kundi lake.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo duniani(FAO)ya mwaka 1999 katika utafiti wake wa ‘Non-wood Forest Product in Tanzania’umebainisha kuwepo kwa wadudu wengi wanaotumika kama kitoweo katika maeneo mbalimbali hapa nchini wakiwemo senene.
Utafiti huo pia unawataja wadudu kama kumbikumbi,swah,nywa na fihwa kuwa mbali na kutumika kama kitoweo pia huzalisha mazao mbalimbali ya chakula.
Hata hivyo senene na aina ya moja ya mchwa warukao wanatajwa kuwa na umuhimu mkubwa katika misitu ya miombo na kuwa wdudu wote hawa huuzwa katika masoko ya ndani baada ya wekewa chunvi na kukaangwa vizuri.
Katika miaka ya hivi karibuni safari ya senene kuelekea mashambani hufupishwa na wafanyabiashara ambao huwekeza pesa nyingi na kuwatega kwa kutumia taa zenye mwanga mkali.Katika eneo la Nyamkazi mjini Bukoba gharama ya kukodi eneo la kuweka mtego wa senene sio chini ya shilingi laki moja na waachuuzi wadogo humlipa ‘mwekezaji’shilingi elfu moja ili waruhusiwe kuokota senene watakaoanguka nje ya pipa lililofungwa taa.
Kwa vyovyote vile changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na ushindani wa kibiashara utakifanya kitoweo cha senene ambacho ni sehemu ya utamaduni wa Wahaya uanze kusahaulika na pengine kubaki kwenye historia tu.
Senene kwa sasa imekuwa ikitumika kama kitega uchumi na hajira ya iana mbili. Kuna ajira ya kundi la Vijana wa Muda na Ajira ya kudumu kwa baadahi ya wajasiamari. Ajira ya muda ni kwa vijana hata ambao sio wahaya wamekuwa wajikiika katika kuwakamata na kuwauza wakati wa msimu tu na kundi la pili ununua senene nyingi amabazo uuzwa kidogo kidogo hadi msimu wa pili unapoanza. Senene zimekuwa zikitumwa kwa njia ya bus, ndege kwa wahaya walioko ndani na nje ya Tanzania hadi huko famle za kiharabu, marekani, ulaya, austaria, Africa kusini na hata Brazil na kuogeza pato kwa wakazi wa Bukoba. Ukweli senene ni wadudu wanaongeza urafiki mkubwa kwani akitumiwa mtu kama zawadi anaweza kukuleta na kukujibu kwa zawadi kubwa mara dufu mfani senene za elfu tano ukimtumia rafiki mpendwa aliye ulaya anaweza kukutumia ngua kama suti yenye dhamaniya zaidi yalaki nane!!
Mazingira yatunzwe vizuri ili wanedlee kuleta neena mkoani kwetu
By William Oswald Rutta
Manager- Kiroyera Tours @2013

No comments:

Post a Comment