Saturday, March 30, 2013

TALII UTAUINUA UCHUMI MKOANI KAGERA



(Na Gilbert J Makwabe)
Fursa za utalii katika mkoa wa Kagera zimebainishwa kuwa nako zipo ambapo baadhi ya watalii wan je na ndani ya nchi wanaonekana kuutembelea hususan wale wa kutoka nchi mbali mbali duniani.

Mkoa wa Kagera ukiwa ni mkoa pekee unaopakana na nchi zote za Africa Mashariki na nchi za maziwa makuu ni hazina kubwa ya nchi ya Tanzania.Mkoa huu umeshuhudiwa kuwa miongoni mwa mikoa yenye hali nzuri ya hewa,mvua za kuaminika,hali nzuri ya uoto wa asili ambapo karibu kila majira ya mwaka uoto wake hubakia ni wa kijani.Kwa hali hiyo ni vigumu sana kuutofautisha mkoa huo na majimbo kama vile Cape town la Afrika Kusini au Rift Valley la huko Kenya kwani ni hali ya kiubaridi baridi na joto la kadiri.Huo ndio mkoa wa Kagera na Mwenyezi Mungu ndivyo alivyouumba mkoa huo.

Tukizirejea taarifa za hivi karibuni kutoka Mamlaka ya Hali ya Hali ya Hewa Tanzania zimeonyesha kuwa kipindi cha mvua za vuli mwaka 2010/2011 ziliongezeka kutoka milimita 80.7 mwezi Augusti 2010 hadi kufikia milimita211.1 mwezi Desemba 2011 sawa na wastani wa milimita 173.42 kwa mwezi. Aidha kwa kipindi cha Januari2012 hadi Mei 2012 mvua ziliongezeka kutoka milimita 94.3 kwa mwezi hadi kufikia milimita 298.18 kwa mwezi.

Taswira hiyo inatuweka katika dhana ya kuwa mkoa kweli unayo matarajio mazuri kwa upatikanaji wa chakula cha kutoasha kwa wananchi na watalii pia,upatikanaji wa maji ya kutosha,malisho ya mifugo na wanyama pori pia. 

Dhana ya utalii mkoani humo imeibuliwa sio muda mrefu uliopita kama mwaka 2002 ambapo kampuni moja ijulikanayo kama Kiroyera tours ilianzishwa kwa madhumuni ya kuanzisha shughuli za kitalii mkoani humo,Tanzania na Afrika Mashariki.

JE,UTALII NI NINI?
Hatuhitaji kukuna sana vichwa kwa kujiuliza swali hilo utalii ni utamaduni wa kutoka sehemu moja na kuitembelea sehemu nyingine,na kwa maana ya utalii katika mada hii nikuwa ni sharti afikiriaye kutalii ajipange kifedha kwanza! Na mtalii huwa na mambo yanayomfanya aweze kutalii,navyo huitwa ni vivutio.Zipo aina nne za vivutio navyo ni VIVUTIO ASILIA ambavyo ni hifadhi za taifa,mkao wa nchi na hali ya hewa.VIVUTIO VILIVYOTENGENEZWA kama mahoteli makubwa,kambi rasmi kwaajili ya wageni,mialo kando ya ziwa au mito,mashamba makubwa kama yale ya miwa,chai majengo mazuri.MATUKIO kama vile uchaguzi mkuu(waangalizi wa kitaifa na kimataifa).AMANI ya nchi.

Ni dhahiri vivutio viingi havijaainishwa mkoani humo lakini vipo ambavyo tayari vimeainishwanavyo ni kama vile Ziwa kongwe kabisa VICTORIA NYANZA upande wake wa magharibi na mialo yake iliyo na maeneo mazuri kabisa ya mchanga mweupe,ukarimu wa wananchi,kisiwa cha Nabesiga,Maeneo ya hija kama vile Nyakijooga,Kishomberwa,msitu wa hifadhi ya taifa Minziro,Uwanja wa mashujaa wa vita vya  

Maeneo mengine ambayo hupendelewa na watalii wafikao mkoani humo ni pamoja na jumba la makumbusho la Bukoba,maporomoko ya maji,Kyamunene hapo pia kuna pango lenye kuhifadhi popo wa ajabu ambao ni nadra sana kuwakuta sehemu nyingine.Hifadhi katika pori la Keza wilayani Ngara,Hifadhi ya wanyama pori ya Biharamulo,mbuga ya wayama Burigi ndani ya mapori hayo wapo wanyama wajulikanao kama  STATUNGA(kama swala)na hawpatikani popote,na wapo pia aina Fulani ya tumbili ambao wataalamu wa wanyama pori wanasema kuwa walitokea nchini Kongo . Mkoa huo pia unamiliki mapori yanayootesha miti ya michongoma na jamii ya miti ijulikanayo kwa kitaalam kama’acacia’ inayopendwa sana na wanyama pori.

Alipohojiwa na mwandishi wa makala haya kuzungumzia juu ya sekta ya utalii mkoani Kagera Meneja wa operesheni za utalii wa hoteli maarufu ya kitalii katika manispaa ya Bukoba,THE WALKGARD HOTELS AND TOURS Bw.Mugashe Leonidas alisema,’utalii ni hobby’ au hulka ya mtu kwani baadhi ya watalii huja mkoani Kagera wakitokea ng’ambo ili pengine kuona maeneo ambayo babu au baba zao waliwahi kufanyia kazi wakati wa ukoloni. Alipoulizwa ni vivutio gani ambavyo ameshuhudia kuweza kuwakosha zaidi watalii wan je ya nchi wafikapo Kagera  aliongeza kuwa ni mashamba ya chai ambapo wao husema kuwa wao huliona tu zao la chai madukani huko kwao lakini kuwa hawajawahi kuliona zao hilo likiwa limeoteshwa shambani.Watalii hupenda sana kupiga picha wakati wakiwa wanaigiza kuvuna chai katika mashamba hayo.
(itaendelea toleo lijalo)

Yapo matatizo yanayoikabili sekta ya utalii mkoani Kagera kama vile hali ya usalama katika mapori ya Biharamulo,Ngara na Karagwe hali ambayo bado inahitaji kudhibitiwa zaidi na huku watalii wakihakikishiwa usalama wawapo ndani ya maeneo hayo.Kutokuwepo kwa uwanja wa ndege wa uhakika hususan wa kimataifa ambao pengine ungeliwasaidia hata mikoa ya nchi jirani ipakanayo na mkoa wa Kagera nayo pia ni Changamoto.Ni busara mradi wa kufikirika wa kutaka kuujenga uwanja huo katika maeneo ya Omukajunguti ukatekelezwa bila kusita.

Mkoa wa kagera hakika unasheheni vivutio vingi ambavyo vingine bado havijabainishwa au hata kutangazwa vya kutosha.Mto Kagera ni chanzo cha mto Nile ambapo duniani kote hamna watu wasiousikia au kuusoma vitabuni mto huo mashuhuri  duniani.Wapo aina wa ndege tofauti tofauti katika vituo vya kuwashuhudia ndege hao na vijito lukuki ambapo watalii wanaweza kufurahia ulowaji samaki ndani ya vijito hivyo pia ypo maji moto Mutagata ya huko wilayani Karagwe.

Alipowasiliana na viongozi wa kampuni(Kiroyera tours) inayoendesha shughuli za utalii mkoani Kagera mwandishi wa makala haya alielezwa jinsi kampuni hiyo inavyoendelea na jitihada za kuutangaza mkoa huo ili nao uweze kuwemo miongoni mwa maeneo maarufu kwa ujio wa watalii nchini Tanzania.

Miongoni mwa juhudi hizo ni kulitangaza ZIWA VICTORIA ambalo ni ziwa kubwa duniani ambalo maji yake siyo ya chumvi na kuwa mtalii anaweza kuingia mkoani Kagera  hatakwa kutumia meli akipitia ndani ya ziwa hilo hadi mjini Bukoba.BUKOBA ni mji unaofikika kirahisi  hata kwa kutokea Nairobi,Kisumu,Mwanza,Kampala,Entebbe,Kigali,,na Bujumbura.Barabara mpya ya lami inayojengwa sasa hivi kutoka Bukoba hadi Wilayani Karagwe itawaunganisha watalii wanaotaka kwenda kuziona hifadhi za taifa za Ibanda na Burigi,majimoto ya Mutagata na kwingineko
Kwa  vile mkoa huo unaweza kufikiwa kirahisi na idadi kubwa ya watalii wanopita kwenda au kutoka nchi jirani ni dhahiri sana iwapo vivutio vile ambavyo bado havijabainishwa vikabainishwa ili watalii hao wakachelewa mkoani humo ili matumizi yao yakahitimishwa mkoani humo pia.
Mkoani Kagera zipo ngoma na michezo asilia kama vile Omutooro,Akasimbo,kutupa mkuki,kuvuta kambangoma za akina mama na nyinginezo.Kwa kuwani jukumu la idara ya Utamaduni kviendeleza vipaji vya aina hiyo,sasa ni wakati wa kuifanya kazi hiyo katika kuwaandaa wananchi wakavuna fedha za watalii pindi waingiapo mkoani humo.

Zoezi endelevu la kuuweka safi mji wa Bukoba a miji mingine ya mkoa wa Kagera chini ya Uongozi wa mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali mstaafu Fabian Massawe ni jambo la kujivunia sana mintarafu sekta ya utalii nchini.Mtalii ni mgeni wa mahali hivyo ni jambo linalosikitisha mno iwapo mgeni huyo anaikuta nyumba yetu ni chafu na haitamaniki.

Kwa hali hiyo panahitajika juhudi zaidi za wananchi hata kuyapiga rangi za kupendeza majengo yetu huku tukiendelea zaidi kuyaboresha mazingira tuishimo.Tunaelezwa na wamiliki wa makampuni ya utalii mkoani Kagera kuwa wageni wanaoutembelea sana mkoa huo ni hasa kutokea nchi za ulaya kaskazini na Afrika kusini. Huko vijijini kwa wale wananchi ambao bado wanazitunza nyumba za asili maarufu kama “MUSHONGE” waendelee kuzihifadhi nyumba hizo kwani huenda hicho kikawa kivutio maalum ambacho bado hakijaainishwa baraabara,kwani utalii si lazima ukaishia mijini tu.

No comments:

Post a Comment