Kwa kutumia vyanzo mbalimbalina
imekuzwa na William Rutta – Kiroyera tours www.kiroyeratours.com
KUNA aina nyingi za wadudu ambao katika baadhi ya makabila hapa nchini
hutumiwa kama kitoweo,na pia katika uzalishaji wa bidhaa za vyakula kwa ajili
ya matumizi mbalimbali.
Senene ambao hupatikana kwa wingi mwishoni mwa kila mwaka, ni miongoni mwa
wadudu wanaotumiwa zaidi na kabila la wahaya mkoani Kagera kama kitoweo,
pengine kuliko kabila jingine unalolifahamu.
Hata hivyo pamoja na kitoweo hiki kupewa heshima kubwa na hata kuwa sehemu
ya mila na utamaduni wa kabila hili,asili na chanzo cha senene limeendelea kuwa
swali gumu miongoni mwa wenyeji wa mkoa huu.
Wahenga walisema ‘uzee dawa’na katika kutafuta majibu ya siri ya senene
katika kabila hili,safari yangu ilinikutanisha na mzee David Zimbihile(80)
aliyekuwa mbunge wa kwanza wa jimbo la Ihangiro sasa ni Muleba Kusini.
Wakati wa uongozi wake alikuwa na mvuto mkubwa kwa wapiga kura,na hadi leo
anakumbukwa kama kiongozi ambaye utawala wake ulikuwa na baraka za wingi wa
senene kila mwaka.
Anasema katika moja ya kampeini zake aliwahi kulalamikia kukosekana kwa
mboga,na badala yake aliomba senene .Sara zake zilisikika na kuanzia wakati huo
wananchi wakaendelea kumwamini huku madai ya uwezo wake wa kuleta senene
yakitumika kutetea nafasi yake.
Mzee Zimbihile anasema pamoja na kupata umaarufu kupitia kitoweo cha senene
miongoni mwa wapiga kura,anasema hakuwa na uwezo huo na kudai aliwaomba na
Mungu akasikia sara zake kutokana na uhaba mkubwa wa mboga uliokuwepo wakati
huo.
Hata hivyo pamoja na kusema senene ni kitoweo kinachoheshimika bado hakuweza
kufahamu asili yake na sababu za wadudu hao kuvutiwa na mazingira ya mkoa wa
Kagera katika misimu miwili kwa mwaka.
Anaamini ni uwezo na mapenzi ya Mungu,huku akikumbuka wakazi wa eneo la
Bunya katika nchi ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) walivyomshanga wakati alipokuwa
wanakamata na kula senene enzi hizo akifanya kazi nchini humo.
Maswali yangu hayakupata majibu na alihitimisha mazungumzo kwa kusisitiza
kuwa tamaa ya kula senene iliwafanya wanaume kuwaongopea wanawake kuwa kama
wangekula kitoweo hicho kingeweza kuwadhuru.
Hata nilipozungumza na Saida Sarehe(67)mkazi wa eneo la Kashai mjini
hapa,alidai hakuna historia yoyote kwenye kabila lao inayoeleza chanzo na asili
ya wadudu hao na kudai Mungu aliitoa kama neema kwa wakazi wa mkoa huo.
Ni muuguzi mstaafu ambaye anaishia kunisimulia jinsi wasichana wa enzi zao
walivyopeleka senene kwa wachumba wao,ambaye hakufanya hivyo ilimaanisha
uwezekano wa kuolewa na mchumba wake ulikuwa mdogo.Senene walitumika kama
ishara ya upendo na uaminifu.
Anasema hawakuruhusiwa kula senene na kudai vitisho vya wanaume
vilivyojificha kwenye tamaa na uroho wa senene viliwafanya wale kitoweo hicho
kwa siri kubwa.
Bila kunipa majibu ya maswali yangu,analalamikia ubabe wa wanaume
uliowakataza kula vitu vitamu na kuanzia hapo ananipa siri ya eneo la mkoa huu
kuitwa Buhaya. Kuna baadhi ya vitu vitamu vingine kama kuku, nyama ya mbuzi,
mayai wakina mama hawakurusiwa kula. Wazee wa kihaya kimila walidai mwanamke
alikuwa haruhisiwi kutmumia vile kizazi kilikua shida na kwa kutumia mayai,
nyama ya mbuzi na kuku wangenenepa na kushindwa kuzaa kwa wepesi ikawa ni
mwiko, Bibi yangu Felista Nyamwiza aliyafariki mwaka 2010 akiwa namika 88
hakuwahi kula senene, yai wala kuku katika maisha yake yote pamoja na
kutuandalia senene sisi wajukuu zake.
Kwamba wanawake walionywa wawe na haya siku zote, na wasivunje mwiko kwa
kula vitu walivyokatazwa.Wote walikuwa na utii wakiheshimu mila na desturi za
kabila lao.Walifundishwa kuwa na haya wasichana wa Buhaya.
Hata Khadija Khalphan(84)mkazi wa Kashai mjini Bukoba mbali na kufahamu
umuhimu na nafasi ya kitoweo cha senene katika mila za kabila lake anakiri
kutofahamu chanzo na asili ya wadudu hao.
Hata mvua za vuli zinazoanza mwezi Novemba ambazo huambatana na ujio wa
senene ,msimu huo hutambuliwa na wenyeji kwa jina la mvua za Omusene ikiwa na
maana halisi ya mvua za msimu wa senene.
Pamoja na senene kuwa ishara ya neema katika kabila hili,pia inadaiwa ni
dalili za kuwepo tukio baya endapo mtu ataota kuona senene wengi.
Juhudi za kufahamu siri ya senene zinanifikisha katika kituo cha Utafiti wa
Kilimo Maruku,na baada ya kushindwa kumpata mtaalamu wa sayansi ya wadudu niliamua
kutafuta majibu kwenye vyanzo mbalimbali kwenye mtandao wa intaneti.
Zipo aina nyingi za senene ambapo wale ninaowazungumzia wamegawanyika katika
kundi lijulikanalo kwa kitaalamu kama Orthopterous na huzaliana kwa wingi
katika mwambao wa maziwa makuu,baada ya kutaga mayai yao ardhini kipindi cha
kiangazi.
Baada ya kutaga mayai na kuanguliwa,mzunguko wa maisha yao huisha kati ya
mwezi Octoba na Desemba ambapo huruka wakiwa katika makundi makubwa
wakihitimisha safari ya maisha yao.
Senene hao ambao wako katika jamii ya nzige pia hutofautiana kutegemea
mazingira yaliyopo na hali ya hewa, na tangu zamani hupenda kuweka makazi yao
juu ya vilima.
Kwa mujibu wa vyanzo vya mtandao katika nchi ya Japan senene wa kijani
humaanisha dalili njema,na mwanzo mzuri wenye matumaini ambapo pia hutumika
katika utengenezaji wa chokoleti.
Hii ni aina ya panzi wapole ambao hawana tabia ya kuharibu mazao na
kuteketeza makazi yao kwa chakula kama walivyo jamii ya nzige.
Hawa ni aina ya panzi ambao baada ya kuzaliana, maisha yao ya mwisho hupenda
kuyamalizia kwenye ukanda wa kijani na bila shaka mkoa wa Kagera ukiwa ni
chaguo bora zaidi.
Senene huanza safari yao wakati wa giza huku pembe zao zikiwa zimeangalia
chini na mara waonapo mapambazuko hujificha chini kwenye nyasi.
Pengine ndiyo sababu wafanya biashara wa senene hufanikiwa kuwahadaa kwa
mwanga mkali wa taa,na mara kadhaa makundi makubwa ya senene huletwa na mawimbi
ya maji baada ya mapambazuko kuwakuta kwenye maeneo ya ziwa Viktoria.
Senene hupatikana mahali pengi duniani ingawa hutofautiana kutokana na
mazingira na ikolojia ya eneo hilo.Madume hutoa mlio maalmu kuwavutia majike
ingawa pia milio hiyo hutofautiana kutokana na aina ya senene na kundi lake.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo duniani(FAO)ya mwaka
1999 katika utafiti wake wa ‘Non-wood Forest Product in Tanzania’umebainisha
kuwepo kwa wadudu wengi wanaotumika kama kitoweo katika maeneo mbalimbali hapa
nchini wakiwemo senene.
Utafiti huo pia unawataja wadudu kama kumbikumbi,swah,nywa na fihwa kuwa
mbali na kutumika kama kitoweo pia huzalisha mazao mbalimbali ya chakula.
Hata hivyo senene na aina ya moja ya mchwa warukao wanatajwa kuwa na umuhimu
mkubwa katika misitu ya miombo na kuwa wdudu wote hawa huuzwa katika masoko ya
ndani baada ya wekewa chunvi na kukaangwa vizuri.
Katika miaka ya hivi karibuni safari ya senene kuelekea mashambani
hufupishwa na wafanyabiashara ambao huwekeza pesa nyingi na kuwatega kwa
kutumia taa zenye mwanga mkali.Katika eneo la Nyamkazi mjini Bukoba gharama ya
kukodi eneo la kuweka mtego wa senene sio chini ya shilingi laki moja na
waachuuzi wadogo humlipa ‘mwekezaji’shilingi elfu moja ili waruhusiwe kuokota
senene watakaoanguka nje ya pipa lililofungwa taa.
Kwa vyovyote vile changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na ushindani wa
kibiashara utakifanya kitoweo cha senene ambacho ni sehemu ya utamaduni wa
Wahaya uanze kusahaulika na pengine kubaki kwenye historia tu.
Senene kwa sasa imekuwa ikitumika kama kitega uchumi na hajira ya iana
mbili. Kuna ajira ya kundi la Vijana wa Muda na Ajira ya kudumu kwa baadahi ya wajasiamari.
Ajira ya muda ni kwa vijana hata ambao sio wahaya wamekuwa wajikiika katika
kuwakamata na kuwauza wakati wa msimu tu na kundi la pili ununua senene nyingi
amabazo uuzwa kidogo kidogo hadi msimu wa pili unapoanza. Senene zimekuwa
zikitumwa kwa njia ya bus, ndege kwa wahaya walioko ndani na nje ya Tanzania
hadi huko famle za kiharabu, marekani, ulaya, austaria, Africa kusini na hata
Brazil na kuogeza pato kwa wakazi wa Bukoba. Ukweli senene ni wadudu wanaongeza
urafiki mkubwa kwani akitumiwa mtu kama zawadi anaweza kukuleta na kukujibu kwa
zawadi kubwa mara dufu mfani senene za elfu tano ukimtumia rafiki mpendwa aliye
ulaya anaweza kukutumia ngua kama suti yenye dhamaniya zaidi yalaki nane!!
Mazingira yatunzwe vizuri ili wanedlee kuleta neena mkoani kwetu
By William Oswald Rutta
Manager- Kiroyera Tours @2013